DERBY YA KARIAKOO YAHAIRISHWA
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha leo Machi 8, 2025 ilipitia shauri la klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo leo kuanzia saa 1:15 usiku.
Katika shauri hilo, klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa hapo juu, huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwasababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo (ambao walishuhudia tukio hilo), kutuma taarifa ya tukio haraka ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi
Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwemo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, Kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba, wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu, haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike.
Katika taarifa hizo, Kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa klabu ya Yanga, walishiriki tukio la kuzuia basi la klabu ya Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kwasababu pia Bodi ilipokea taarifa ya Ofisa Usalama wa mchezo ambayo imeainisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi, na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati, Bodi ya Ligi kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1(1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.
Bodi itatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo na kutangaza tarehe ya mchezo huo mapema iwezekanavyo.
#SimbaSC #YangaSC #KariakooDerby #LigiKuu #FootballTanzania #WataniWaJadi #bodiyaligi #tanfootball