Mchungaji Mashimo Ahukumiwa Miaka Miwili Jela Kwa Kuharibu Nyumba

Mchungaji Mashimo Ahukumiwa Miaka Miwili Jela Kwa Kuharibu Nyumban
Mchungaji Mashimo Ahukumiwa Miaka Miwili Jela Kwa Kuharibu Nyumba

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela Mchungaji Daud Nkuba, maarufu kama Komando Mashimo au Nabii Mikaya, baada ya kupatikana na hatia ya kuharibu ujenzi wa nyumba mali ya Frola Mwashaa katika eneo la Mbezi Luis, Dar es Salaam.

Aidha, Mahakama imemtia hatiani kwa kuingia kwa jinai katika ardhi ya Frola Mwashaa, lakini imemuachia huru katika shtaka la kutishia kwa vurugu, kwa kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shtaka hilo bila shaka yoyote.

Hukumu hiyo imesomwa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, ambaye amesema upande wa mashtaka umethibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa kupitia mashahidi watano na vielelezo mbalimbali "Kwa shtaka la kuingia kwa jinai, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miezi sita, na kwa kosa la kuharibu mali, atatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani," alisema Hakimu Rugemalira.

Hata hivyo, Mahakama imeamua vifungo hivyo viende kwa pamoja, hivyo Komando Mashimo atatumikia kifungo cha miaka miwili pekee.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Rhoda Kamungu, aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Komando Mashimo aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu, akidai ana familia inayomtegemea.

Komando Mashimo alishtakiwa kwa makosa matatu:

Kuingia kwa jinai katika ardhi ya Frola Mwashaa mnamo Novemba 22, 2023, eneo la Mbezi Luis, Wilaya ya Ubungo.

Kuharibu ujenzi wa nyumba ya Frola Mwashaa kinyume cha sheria.

Kutishia kwa vurugu dhidi ya Ramson Vicent – shtaka hili lilikosa ushahidi wa kutosha, hivyo Mahakama ikamuachia huru.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post